Mgogoro mkubwa umeibuka ndani ya klabu ya Real Madrid baada ya kiungo Dani Ceballos kuingia kwenye mvutano mkali na kocha Álvaro Arbeloa, hali iliyofikia hatua ya kuvunjika kabisa kwa uhusiano wao.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka gazeti la Marca, Ceballos hataitwa tena kwenye kikosi cha mechi hadi mwisho wa msimu, huku Arbeloa akidaiwa “hataki hata kumuona” mchezaji huyo.
Tukio hilo linafuatia kikao cha ana kwa ana kilichofanyika mazoezini Valdebebas, ambapo mazungumzo yaligeuka kuwa mabaya na kuashiria mwisho wa uhusiano wao .
Inaelezwa kuwa baada ya kikao hicho, Ceballos aliwaambia wachezaji wenzake wazi kuwa hataki tena kuwa na mawasiliano yoyote na kocha wake, kauli iliyothibitisha kuwa mgogoro huo umefikia hatua ya “hakuna kurudi nyuma” .
Hali hiyo imeathiri moja kwa moja nafasi yake uwanjani. Licha ya kuwa fiti, kiungo huyo amekuwa akiachwa nje ya kikosi katika mechi muhimu za La Liga, jambo lililozua maswali mengi kwa mashabiki.
Ndani ya klabu, uongozi unaonekana kusimama upande wa kocha, ukiuchukulia uamuzi huo kama wa kiufundi, lakini ukweli ni kwamba uhusiano wao umevunjika kabisa .
Kwa sasa, ishara zote zinaonyesha kuwa huu ndio mwisho wa safari ya Ceballos katika Santiago Bernabéu. Licha ya kuwa na mkataba unaoendelea hadi 2027, mipango iliyopo ni wazi, ataondoka majira ya kiangazi kutafuta changamoto mpya, huku klabu ya zamani ya Real Betis ikitajwa kama moja ya chaguo lake kuu .



