Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba SC Ahmed Ally, ametoa taarifa nzuri kwa mashabiki wa timu hiyo kuhusu hali ya majeruhi wake kuelekea mchezo mkubwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Young Africans SC, maarufu kama dabi ya Kariakoo.
Mchezo huo unatarajiwa kupigwa Jumapili, Mei 03, katika uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, ukiwa ni moja ya mechi zinazovuta hisia kubwa zaidi katika soka la Tanzania.
Wote wako fiti kwa dabi
Ahmed Ally amethibitisha kuwa nyota watatu muhimu wa kikosi hicho, Anicet Oura, Nickson Kibabage na Yusuph Kagoma wote wamepona majeraha waliyoyapata katika mchezo uliopita wa fainali ya Kombe la Muungano na sasa wako tayari kuanza mazoezi pamoja na kikosi.
Wachezaji hao walishindwa kumaliza mchezo huo kutokana na matatizo ya majeraha, hali iliyoibua hofu kwa mashabiki wa Simba kuhusu uwezekano wao kukosa dabi hiyo muhimu.
Kauli ya Ahmed Ally
Akizungumza kuhusu hali ya kikosi, Ahmed Ally alisema:
"Napenda kuwajulisha kwamba wachezaji wote (Oura, Kibabage na Kagoma) ambao walitolewa katika mchezo wa fainali ya Kombe la Muungano kwa kuumia, wote wako tayari kwa mchezo wa Jumapili. Ninapozungumza hapa wachezaji wapo vizuri kabisa. Cha kufanya ni kumuomba Mwenyezi Mungu aendelee kulinda hali zao."
Simba kuingia kambini
Simba SC iliingia kambini rasmi jana kuanza maandalizi ya mwisho ya mchezo huo muhimu dhidi ya watani wao wa jadi. Timu hiyo inaendelea kujifua kwa kasi kubwa ikiwa na lengo la kuhakikisha inapata matokeo chanya katika moja ya michezo migumu zaidi ya msimu.
Dabi hiyo ya Kariakoo inatarajiwa kuwa na ushindani mkali, huku pande zote mbili zikihitaji ushindi kwa malengo tofauti ya msimamo wa ligi.
Simba inahitaji ushindi ili kupunguza gap la pointi dhidi ya watani zao Yanga kuwa 2 ili kusalia katika vita ya kuwania ubingwa.



