Yanga, Simba watambiana kuelekea fainali ya Kombe la Muungano

Joel JJ By Joel JJ • 27th April 2026


Yanga, Simba watambiana kuelekea fainali ya Kombe la Muungano

Mvutano wa maneno kati ya vigogo wa soka la Tanzania, Yanga na Simba SC, unazidi kupamba moto kuelekea fainali ya Kombe la Muungano itakayopigwa Jumatano, Aprili 29 katika Uwanja wa New Amaan Complex.

Juzi Yanga ilikuwa ya kwanza kutinga fainali kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Azam FC, kabla ya Simba kuungana nao kufuatia ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Mlandege FC katika nusu fainali ya pili.

Kamwe atamba: “Simba wameingia kwenye mtego”

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, amesema klabu hiyo imefurahishwa na Simba kutinga fainali, akidai kuwa wapinzani wao wameingia katika “mtego” waliokuwa wameuandaa.

Kamwe amesema Yanga ilitamani kukutana na Simba kabla ya mchezo wa ligi kuu na sasa jambo hilo limetimia.

“Sisi tumefurahi kwa wao kuingia fainali kwani mitego yetu sasa imetimia,” alisema Kamwe.

Yanga na Simba tayari zimekutana mara mbili msimu huu. Mchezo wa Ngao ya Jamii uliishia Yanga kushinda 1-0, kabla ya sare tasa ya 0-0 katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa New Amaan Complex.

Simba wajibu mapigo kwa tambo

Kwa upande wa Simba, Meneja wa Habari na Mawasiliano Ahmed Ali amesema klabu hiyo iko tayari kwa mapambano ya “kulipa kisasi” dhidi ya Yanga katika mechi mbili mfululizo fainali ya Muungano Cup na mchezo wa ligi kuu utakaofuata Mei 3.

Ahmed amefichua pia kuwa Simba walitamani kukutana na Yanga fainali, na hata waliombea Azam FC ifungwe ili mpambano huo mkubwa utimie.

“Sisi tunapenda kucheza mechi kubwa na tulipiga goti kwa Mungu tukiomba Azam FC wafungwe na Yanga,” alisema Ahmed.

Historia mpya ya ushindani

Mvutano huu unakuja katika mazingira ambayo Yanga wameonekana kuimarika zaidi tangu walipokutana mara ya mwisho Machi 1, baada ya maboresho ya benchi la ufundi hasa ujio wa kocha msaidizi Abdulhamid Moalin, ambapo timu hiyo imekuwa ikipata matokeo chanya mfululizo.

Kwa upande wa Simba, ushindi wao wa nusu fainali dhidi ya Mlandege FC umeonyesha ubora wa kikosi chao, wakiamini sasa wako tayari kutwaa taji la Muungano mbele ya Yanga

Fainali ya presha na heshima

Fainali ya Kombe la Muungano sasa inatarajiwa kuwa zaidi ya mchezo wa kawaida, ni vita ya heshima, ubabe na kisa cha kisasi kati ya wapinzani hawa wakubwa wa soka la Tanzania.

Baada ya hapo, timu hizo zitakutana tena Mei 3 katika mchezo wa ligi kuu,  mashabiki watashuhudia “wiki ya moto” ya dabi ya Kariakoo.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.