Simba kuifuata Yanga fainali Muungano Cup leo?

Joel JJ By Joel JJ β€’ 26th April 2026


Simba kuifuata Yanga fainali Muungano Cup leo?

Kikosi cha Simba SC kinatarajiwa kushuka dimbani leo Jumapili katika Uwanja wa New Amaan Complex kuikabili Mlandege FC katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Muungano, ukiwa ni mtihani muhimu utakaopamua hatma ya safari yao kuelekea fainali.

Ni dakika 90 za maamuzi kwa Wekundu wa Msimbazi, ambapo ushindi pekee utawatosha kuwapeleka moja kwa moja fainali ya mashindano hayo ya kihistoria.

Simba inakabiliwa na presha ya matokeo mazuri hasa ikizingatiwa kuwa tayari Young Africans SC wameshaingia fainali baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Azam FC katika nusu fainali nyingine iliyopigwa jana.

Matokeo ya Yanga yameweka presha zaidi kwa Simba, kwani ushindi wa leo utamaanisha fainali ya Kombe la Muungano itakuwa dabi ya Kariakoo kati ya mahasimu hao wakubwa wa soka nchini.

Kocha mkuu wa Simba, Steve Barker, jana alionekana Uwanja wa New Amaan Complex akishuhudia nusu fainali ya kwanza kati ya Azam FC na Yanga, hatua inayoaminika kuwa sehemu ya maandalizi ya kimkakati kuelekea mchezo wa leo.

Uwepo wake uwanjani ulionekana kama fursa ya kujipima na kupanga mbinu za kukabiliana na moja ya timu hizo endapo Simba itafuzu fainali.

Zaidi ya nusu fainali hiyo, matokeo ya leo yanaongeza uzito wa ratiba, kwani endapo Simba itashinda, itakutana tena na Yanga katika fainali, kabla ya timu hizo kurudi tena kwenye ligi kuu Mei 3 katika mchezo mwingine mkubwa utakaopigwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Stadium.

Mchezo huo wa ligi kuu unatarajiwa kuwa na hisia kali zaidi kutokana na ushindani wa timu hizo kuwania ubingwa wa ligi kuu msimu huu.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.