Real Madrid yazidi kupotea njia ubingwa La Liga

Joel JJ By Joel JJ • 25th April 2026


Real Madrid yazidi kupotea njia ubingwa La Liga

Klabu ya Real Madrid imeendelea kupoteza mwelekeo katika mbio za ubingwa wa La Liga baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya Real Betis, katika mchezo uliochezwa Ijumaa usiku.

Katika mchezo huo uliopigwa jijini Sevilla, Madrid walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia nyota wao Vinícius Júnior aliyefunga mapema dakika ya 17, akimalizia vizuri shambulizi lililoanzishwa na Federico Valverde.

Hata hivyo, pamoja na kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga mabao zaidi zikiwemo juhudi za Jude Bellingham na Kylian Mbappé, Madrid walishindwa kuongeza bao la pili, jambo lililowapa nafasi wapinzani wao kurejea mchezoni.

Dakika za lala salama, beki wa Betis Héctor Bellerín aliisawazishia timu yake bao muhimu dakika ya 93, akitumia uzembe wa safu ya ulinzi ya Madrid.

Matokeo hayo yamekuwa pigo kubwa kwa Real Madrid katika mbio za ubingwa, kwani sasa wanabaki nyuma kwa alama nane dhidi ya vinara wa ligi, huku wapinzani wao wakubwa FC Barcelona wakiwa na mchezo mkononi, hali inayoweza kuongeza pengo hilo hadi alama 11.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa soka, sare hiyo imeifanya safari ya Madrid kuelekea ubingwa kuwa ngumu zaidi, huku presha sasa ikielekezwa kwenye mchezo ujao mkubwa wa El Clásico, ambao unaweza kuamua hatma ya mbio hizo.

Kwa upande wa Real Betis, matokeo hayo ni mafanikio makubwa dhidi ya timu yenye hadhi ya juu kama Madrid, huku wao wakiendelea kupambania nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.