Sakata kati ya klabu ya Yanga na vyombo vya habari vya EFM na TVE limechukua sura mpya kufuatia maudhui yaliyorushwa Aprili 17, 2026 kwenye kipindi cha michezo cha Namba 10. Maudhui hayo, yaliyotolewa na mchambuzi Wilson Oruma maarufu kama >Mzee wa Jambia, yameibua mjadala mkubwa miongoni mwa wadau wa soka nchini.
Akizungumza na wanahabari, Mkuu wa Idara ya Michezo wa EFM na TVE, Abbisay Stephen Jr, alieleza kuwa Aprili 20 walipokea barua kutoka kwa Mwanasheria wa klabu ya Yanga. Barua hiyo ilieleza kusudio la kuchukua hatua za kisheria dhidi ya taasisi hiyo kwa madai ya kashfa na uchochezi uliodaiwa kufanywa kupitia kauli za mchambuzi huyo.
Abbisay alisisitiza kuwa EFM na TVE hazina utaratibu wa kurusha maudhui chonganishi au yasiyo na mizania ya ushahidi. Alifafanua kuwa kauli zote zilizotolewa na Oruma zilikuwa ni maoni yake binafsi na si msimamo rasmi wa kituo hicho.
βNi kosa kutumia jukwaa letu kinyume na taratibu zinazofahamika. Tayari tumeshachukua hatua mbalimbali, ikiwemo kufuta maudhui yote husika na kumtaka mhusika kuomba radhi kupitia majukwaa yetu,β alisema Abbisay.
Hata hivyo, jitihada za kumtaka Oruma aombe radhi zimegonga mwamba, baada ya mchambuzi huyo kugoma kufanya hivyo. Kwa mujibu wa Abbisay, Oruma amesimama kidete akieleza kuwa yuko tayari kwenda mahakamani kujitetea.
Uamuzi huo umeongeza mvutano katika sakata hilo, huku klabu ya Yanga tayari ikithibitisha kufungua shauri mahakamani dhidi ya mchambuzi huyo. Hatua hii inaashiria kuwa mgogoro huo sasa umeingia katika hatua ya kisheria, na hatima yake huenda ikaamuliwa na vyombo vya sheria.



