Italia yapigiwa chapuo ichukue nafasi ya Irani kombe la Dunia 2026

Joel JJ By Joel JJ • 23rd April 2026


Italia yapigiwa chapuo ichukue nafasi ya Irani kombe la Dunia 2026

Pendekezo la kuitaka FIFA kuiondoa Iran na nafasi yake kuchukuliwa na Italia katika fainali za FIFA World Cup 2026 limezua mjadala mkubwa katika ulimwengu wa soka na siasa.

Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na gazeti la Financial Times, Paolo Zampolli, mjumbe wa Donald Trump, amethibitisha kuwasilisha pendekezo hilo kwa Rais huyo wa Marekani pamoja na Rais wa FIFA, Gianni Infantino.

“Nimependekeza kwa Trump na Infantino kuwa Italy ichukue nafasi ya Iran. Ni ndoto kuona Azzurri ikicheza Kombe la Dunia linalofanyika Marekani,” alinukuliwa Paolo Zampolli akieleza, akisisitiza historia ya Italia yenye mataji manne ya dunia.

Taarifa zinaeleza kuwa mpango huo unahusishwa pia na juhudi za kurekebisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Donald Trump na Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni.

Inaelezwa kuwa uhusiano huo uliwahi kuzorota kufuatia kauli za Trump katika muktadha wa mvutano wa kimataifa unaohusisha Iran, hali iliyochochea mjadala wa kisiasa kuingia katika masuala ya michezo.

Hakuna uamuzi rasmi FIFA

Pamoja na mjadala huo, FIFA haijatoa tamko lolote rasmi la kuiondoa Iran kwenye mashindano hayo.

Iran tayari imefuzu kushiriki FIFA World Cup 2026 kupitia michuano ya kufuzu ya bara la Asia na inaendelea na maandalizi kama kawaida kuelekea fainali hizo zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico.

Kwa upande wa Italia, timu hiyo ilishindwa kufuzu baada ya kupoteza kwa mikwaju ya penalti 4-1 dhidi ya Bosnia and Herzegovina katika hatua ya mchujo wa Ulaya, hivyo kubaki nje ya mashindano hayo.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.