Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetangaza rasmi kuanza kwa mchakato wa kupokea maoni ya maboresho ya Kanuni za Ligi kwa toleo la mwaka 2026, hatua inayolenga kuboresha uendeshaji wa mashindano ya mpira wa miguu nchini.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, maoni na mapendekezo yanayokusanywa yatahusisha Kanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara, Ligi ya Championship pamoja na First League. Mchakato huu unalenga kuhakikisha kanuni zinakuwa bora zaidi na zinaendana na mazingira ya sasa ya ushindani wa soka nchini.
TPLB imesisitiza kuwa lengo kuu la zoezi hili ni kuboresha kanuni ili ziweze kutoa majibu kwa changamoto zilizojitokeza na zile zinazoweza kujitokeza katika msimu wa 2025/2026. Hatua hii pia inalenga kuongeza uwazi, ufanisi na ushindani wa haki katika ligi zote zinazosimamiwa na bodi hiyo.
Mchakato wa kupokea maoni umefunguliwa rasmi tarehe 22 Aprili 2026 na utadumu kwa kipindi cha wiki nne. Bodi hiyo imewahimiza wadau wote wa soka, ikiwa ni pamoja na vilabu, viongozi, waamuzi, wachezaji na wadau wengine, kushiriki kikamilifu katika kutoa mapendekezo yao.
TPLB imekumbusha kuwa kanuni bora ni msingi muhimu wa kuwa na ligi imara na yenye maendeleo chanya kwa mpira wa miguu kwa ujumla nchini Tanzania. Ushiriki wa kila mdau unatajwa kuwa ni muhimu katika kuhakikisha maboresho yanayofanyika yanaakisi mahitaji halisi ya mchezo.
Maoni ya maboresho ya kanuni yanatakiwa kuwasilishwa TPLB kabla ya tarehe 22 Mei 2026 kupitia njia rasmi zitakazotangazwa na Bodi ya Ligi.



