Klabu ya Singida BS imejitokeza na kutoa msimamo wake kuhusu mvutano unaoendelea kati ya Yanga na baadhi ya wachambuzi wa soka nchini, ikisisitiza umuhimu wa kulinda heshima ya klabu na taswira ya ligi kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi kabla ya kuelekea Zanzibar, msemaji wa Singida BS, Hussein Massanza, ameipongeza Yanga SC kwa kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya watu wanaodaiwa kutoa tuhuma na kauli zinazolenga kuichafua klabu hiyo.
Massanza amesema Singida BS pia imekuwa ikikumbana na tuhuma zisizo na msingi, ikiwemo madai kwamba klabu hiyo ina uhusiano wa upendeleo na Yanga SC au kwamba ipo Ligi Kuu kwa ajili ya kuisaidia klabu hiyo.
Amesisitiza kuwa taarifa hizo hazina ukweli na zinapaswa kupuuzwa, huku akibainisha kuwa endapo zitaendelea, klabu haitasita kuchukua hatua za kisheria.
Aidha, Singida BS imeeleza kuwa hatua iliyochukuliwa na Yanga SC ya kufikisha suala hilo kwenye vyombo vya sheria ni mfano wa kuigwa, kwani inalenga kulinda heshima ya klabu, ligi na taswira ya soka la Tanzania kwa ujumla.
Klabu hiyo pia imezitaka timu nyingine zinazokutana na changamoto za aina hiyo kuchukua hatua kama hizo badala ya kukaa kimya, ikisisitiza kuwa baadhi ya wachambuzi wamekuwa wakitoa kauli zinazoweza kuchafua klabu na kuathiri maendeleo ya mchezo.
"Yanga wamefanya jambo zuri kulipeleka mahakamani suala linalofanana na hilo kwani tuhuma za namna hiyo haziishii kuchafua klabu tu bali pia zinachafua Ligi na vyombo vyote vinavyosimamia soka kiujumla."
"Ni vyema timu zote zinazokutana na changamoto za namna hiyo zichukue hatua kama zilizochukuliwa na Yanga kwani wapo wachambuzi ambao wanazichafua klabu nyingine pia," alisema Massanza.



