Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kupitia Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi katika kikao chake cha tarehe 18 Aprili, 2026, kuhusu matukio mbalimbali ya Ligi na maamuzi yaliyofikiwa:
Maamuzi ya Ligi Kuu ya NBC
1. Mechi Namba 07: TRA United FC 0-0 Simba SC
Adhabu: Vilabu vya TRA United na Simba SC vimetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kila kimoja.
Kosa: Walinzi wa klabu hizo (Stewards) kupigana mara baada ya timu kuwasili kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Kanuni: 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
2. Mechi Namba 132: Pamba Jiji FC 0-3 Young Africans SC
Adhabu: Mchezaji Mudathir Yahya (Young Africans) amefungiwa michezo mitatu (3) na kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja).
Kosa: Kumpiga kiwiko mchezaji wa Pamba Jiji, Ibrahim Abraham, mchezo ukiwa unaendelea kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Kanuni: 41:5(5.2) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
3. Mechi Namba 146: Coastal Union FC 1-1 Mtibwa Sugar FC
Adhabu: Klabu ya Coastal Union imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano).
Kosa: Mashabiki wake kurusha chupa za maji uwanjani wakati waamuzi wakiwatuliza Victor Collins (Mtibwa Sugar) na Athuman Makambo (Coastal Union) baada ya Victor kumsukuma Makambo.
Kanuni: 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
4. Mechi Namba 151: TRA United 2-0 Singida BS
Adhabu: Klabu ya Singida BS imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano).
Kosa: Viongozi wake wawili kuingia uwanjani na kumwaga viminimika, jambo lililotafsiriwa kama imani za kishirikina kabla ya timu kupasha moto misuli.
Kanuni: 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
5. Mechi Namba 152: Azam FC 0-0 Simba SC
Adhabu kwa Azam FC: Imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano).
Kosa: Viongozi wa benchi la ufundi na wachezaji kutumia mlango usio rasmi kuingia uwanjani kinyume na kanuni na makubaliano ya kikao cha maandalizi (Pre-match meeting).
Kanuni: 17:21 na 17:62 kuhusu Taratibu za Mchezo.
Adhabu kwa Simba SC: Imetozwa faini ya Sh. 10,000,000 (milioni kumi).
Kosa: Mashabiki wake kumrushia chupa za maji mwamuzi msaidizi namba mbili baada ya kuonyesha kibendera kuashiria mchezaji wa Simba ameotea (offside).
Maelezo ya ziada: Hili ni kosa la kujirudia kwa klabu ya Simba msimu huu (2025/2026), ambapo mashabiki walishafanya kosa kama hilo katika michezo miwili tofauti awali.
Kanuni: 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.



