Sundowns yatangulia fainali ligi ya mabingwa baada ya ushindi dhidi ya Esperance

Joel JJ By Joel JJ • 18th April 2026


Sundowns yatangulia fainali ligi ya mabingwa baada ya ushindi dhidi ya Esperance

Klabu ya Mamelodi Sundowns imefanikiwa kutinga fainali ya CAF Champions League 2026 baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Espérance Sportive de Tunis katika mchezo wa mkondo wa pili wa nusu fainali uliopigwa katika Uwanja wa Loftus Versfeld Stadium.

Ushindi huo umeifanya Sundowns kufuzu kwa jumla ya mabao 2-0, kufuatia ushindi wa 1-0 walioupata ugenini nchini Tunisia katika mchezo wa kwanza uliochezwa Aprili 12, 2026.

Bao pekee la mchezo wa leo lilifungwa na mshambuliaji Brayan León, aliyefunga kwa kufuatilia mpira wa kurejea baada ya penalti yake kuokolewa na kipa wa Esperance.

Katika mchezo huo, Sundowns walionyesha nidhamu ya hali ya juu wakitumia vyema nafasi zao chache za kufunga huku wakijipanga imara katika safu ya ulinzi kuzuia mashambulizi ya wapinzani wao.

Licha ya Esperance kuongeza presha hasa katika kipindi cha pili, walishindwa kupata bao kutokana na ukosefu wa umakini katika umaliziaji.

Kwa matokeo hayo, Sundowns wamefanikiwa kufika fainali ya mashindano hayo kwa mara ya tano katika historia yao, baada ya kufika hatua hiyo mwaka 2001, 2016, 2024, 2025 na sasa 2026.

Katika hatua ya fainali, Sundowns watakutana na mshindi kati ya klabu za Morocco, RSB Berkane na AS FAR Rabat, katika michezo miwili itakayochezwa Mei 15 na Mei 24, 2026.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.