Klabu ya Simba SC imeanza mchakato wa kumbakisha mshambuliaji wake Suleiman Mwalimu ambaye mkataba wake wa mkopo unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.
Kwa mujibu wa makubaliano ya awali, Mwalimu atarejea katika klabu yake mama ya Wydad AC mwezi Juni mara baada ya mkataba wake wa mkopo kumalizika.
Hata hivyo, uongozi wa Simba umeanza mapema harakati za kuhakikisha mshambuliaji huyo anabaki Msimbazi kwa msimu mwingine, kutokana na mchango wake mkubwa ndani ya kikosi.
Taarifa zinaeleza kuwa klabu hiyo inapendelea ama kumsajili moja kwa moja au kumwongezea mkopo mwingine, endapo dili la ununuzi wa moja kwa moja litashindikana.
Hatua hiyo imechochewa na kiwango bora cha Mwalimu msimu huu, ambapo amekuwa mchezaji tegemeo katika safu ya ushambuliaji.
Mshambuliaji huyo, amekuwa na msimu mzuri akiwa kinara wa mabao ndani ya Simba, akifunga jumla ya mabao 6 katika Ligi Kuu ya NBC.
Kocha wa Simba, Steve Barker, anamtegemea Mwalimu katika mfumo wake wa ushambuliaji, akimuona kama sehemu muhimu ya “project” ya msimu ujao.
Inaelezwa mpango wa Simba ni kuhakikisha wanakamilisha dili hilo mapema ili kuepuka ushindani kutoka kwa klabu nyingine zinazoweza kuvutiwa na kiwango cha mchezaji huyo.
Kwa mujibu wa taarifa, hatua hii imechukuliwa mapema pia kutokana na taarifa zinazoibuka kwamba mabingwa wa soka Tanzania Bara Yanga nao wamekuwa na mawasiliano na Wydad wakilenga kumsajili Mwalimu.
Kitendo cha Mwalimu juzi kuonekana uwanja wa KMC Complex wakati Yanga ikichuana na Mbeya City kwenye mchezo wa ligi kuu ya NBC kimeibua mijadala mingi mitandaoni juu ya mustakabali wake.
Hata hivyo nyota huyo alitumia muda wake wa mapumziko akiambatana na marafiki zake kwenda kushuhudia mchezo huo. Kocha wa Simba Steve Barker aliwapa wachezaji wake mapumziko baada ya kurejea Dar kutoka Arusha walikocheza mchezo wa ligi kuu dhidi ya Fountain Gate



