Kocha na nyota wa zamani wa Chelsea Fc Frank Lampard ameiongoza Coventry City kurejea katika Premier League kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 25, kufuatia msimu mzuri wa ligi ya EFL Championship.
Coventry ilithibitisha kupanda daraja baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Blackburn Rovers katika mchezo uliochezwa Ijumaa usiku. Matokeo hayo yaliihakikishia timu hiyo alama 86 ambazo haziwezi kufikiwa na wapinzani wao wa karibu katika msimamo wa ligi.
Bao la kusawazisha lililofungwa dakika za mwisho lilizua shangwe kubwa kwa mashabiki wa Coventry, ambao wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu kurejea katika ligi kuu tangu waliposhuka daraja mwaka 2001.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Lampard alisema mafanikio hayo ni matokeo ya kazi kubwa na mshikamano wa timu nzima. “Hii ni siku muhimu kwa klabu. Wachezaji wameonyesha moyo wa kipekee na wanastahili mafanikio haya,” alisema kocha huyo.
Coventry City imepitia kipindi kigumu katika miaka ya nyuma, ikiwahi kushuka hadi madaraja ya chini kabla ya kuanza safari ya kurejea juu taratibu. Kupanda kwao daraja kunatajwa kuwa moja ya mafanikio makubwa katika historia ya hivi karibuni ya klabu hiyo.
Kwa upande mwingine, mafanikio hayo yanampa nafuu Lampard ambaye amewahi kukumbana na changamoto katika vipindi vyake vya ukocha katika vilabu mbalimbali nchini England. Ushindi huu sasa unaongeza uzito katika wasifu wake kama kocha.



