Kocha wa Arsenal FC, Mikel Arteta, ameibua mjadala mkubwa baada ya kufichuliwa kwa mbinu zake zisizo za kawaida za kuwaandaa wachezaji wake kisaikolojia kabla ya mechi muhimu.
Kwa mujibu wa ripoti ya The Athletic, Arteta aliwahi kuwasha moto halisi katika uwanja wa mazoezi wa London Colney kama sehemu ya kuwajengea wachezaji wake hisia ya “kuwa moto” kabla ya pambano lao dhidi ya Sporting CP katika UEFA Champions League.
Inaelezwa kuwa kabla ya mechi hiyo, Arteta alizungumza na wachezaji wake kuhusu umuhimu wa kuingia uwanjani wakiwa na ari ya hali ya juu, lakini badala ya kubaki kwenye maneno tu, aliamua kuonesha hali hiyo kwa vitendo, hatua iliyowashangaza wengi ndani ya kikosi.
Hii si mara ya kwanza kwa Arteta kutumia mbinu za kipekee za kisaikolojia. Awali aliwahi kutumia vielelezo vya picha za wanyama kama mbwa mwitu ili kuhamasisha umoja na ari ya ushindani ndani ya timu. Mbinu hizo zina lengo la kuwafanya wachezaji “kuhisi” zaidi kuliko kusikia tu maelekezo ya kawaida ya kiufundi.
Wapo wanaoona hatua hizo kama ubunifu unaochangia mafanikio ya timu, hasa ikizingatiwa kuwa Arsenal wamefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya Champions League. Hata hivyo, wengine wanaibua maswali kuhusu usalama na ufanisi wa mbinu hizo kwa kila mchezaji.
Licha ya mjadala huo, matokeo ya uwanjani yanaonekana kuipa nguvu falsafa ya Arteta, ambaye anaamini kuwa mafanikio ya soka hayaanzi tu kwa mbinu za kiufundi bali pia katika maandalizi ya kisaikolojia ya wachezaji.
Kwa sasa, Arsenal wanaendelea na safari yao ya Ulaya wakiwa na matumaini makubwa, huku mbinu za Arteta zikiendelea kuwa sehemu ya mjadala mkubwa ndani na nje ya uwanja, hususani katika mechi inayowakabili mbeleni dhidi ya Manchester City.



