Gwiji wa soka duniani, Lionel Messi, amefungua ukurasa mpya katika maisha yake nje ya uwanja baada ya kuthibitishwa kuwa mmiliki mpya wa klabu ya Hispania, UE Cornellà.
Taarifa kutoka Hispania zinaeleza kuwa Messi amenunua asilimia 100 ya hisa za klabu hiyo inayoshiriki ligi ya daraja la tano nchini Hispania .
Klabu hiyo yenye makazi yake Catalonia, karibu na jiji la Barcelona, imeeleza kuwa ujio wa Messi unaashiria mwanzo wa enzi mpya yenye malengo ya kukuza vipaji vya vijana, kuimarisha miundombinu ya klabu, na kujenga mafanikio ya muda mrefu.
Hatua hiyo pia inaonekana kuimarisha zaidi uhusiano wa Messi na eneo la Catalonia, ambako alijijengea jina kubwa akiwa mchezaji wa FC Barcelona kwa miaka mingi.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, uwekezaji huo si wa kifedha pekee, bali unaambatana na mpango wa kimkakati wa kuendeleza soka la vijana na kuifanya klabu kuwa imara kiushindani na kiutawala kwa muda mrefu.
UE Cornellà inajulikana kwa historia yake ya kukuza vipaji, ikiwa imewahi kutoa wachezaji waliokuja kung’ara Ulaya kama Jordi Alba na David Raya.
Hatua ya Messi inaongeza orodha ya mastaa wa soka wanaoingia kwenye umiliki wa vilabu, ikiwa ni maandalizi ya maisha baada ya kucheza na njia ya kuacha urithi mkubwa zaidi ndani ya mchezo huo.



