Sundowns wauza tiketi zote kuelekea mchezo dhidi ya Esperance Jumamosi

Joel JJ By Joel JJ • 16th April 2026


Sundowns wauza tiketi zote kuelekea mchezo dhidi ya Esperance Jumamosi

Tiketi zote zimeuzwa kuelekea mchezo wa marudiano wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Mamelodi Sundowns na Espérance Sportive de Tunis utakaochezwa Jumamosi, Aprili 18, Loftus Versfeld jijini Pretoria.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi za klabu, uwanja unatarajiwa kujaa mashabiki, hali inayoashiria presha kubwa na ushindani mkali katika pambano hilo la kuwania tiketi ya kucheza fainali ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika.

Mamelodi Sundowns wanaingia katika mchezo huo wakiwa na faida ya ushindi wa bao 1-0 walioupata katika mchezo wa kwanza uliochezwa nchini Tunisia, matokeo yanayowaweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele iwapo wataepuka kupoteza nyumbani.

Pamoja na hilo, Esperance wanatarajiwa kutoa upinzani mkali wakitumia uzoefu wao mkubwa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wakiwa miongoni mwa vilabu vyenye mafanikio makubwa katika historia ya michuano hiyo.

Matarajio ya mashabiki ni makubwa huku mazingira ya mchezo yakitajwa kuwa ya kipekee kutokana na hamasa iliyojitokeza baada ya tiketi kuuzwa mapema, jambo linalotarajiwa kuongeza msukumo kwa wenyeji na kuleta changamoto kwa wageni.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.