Yanga yafungua gap la Alama 5 baada ya viporo kukamilika

Joel JJ By Joel JJ β€’ 15th April 2026


Yanga yafungua gap la Alama 5 baada ya viporo kukamilika

Baada ya kukamilika kwa mechi za viporo za Ligi Kuu NBC, sasa pazia la mzunguko wa 18 limefungwa rasmi huku baadhi ya timu zikianza tayari harakati za mzunguko wa 19.

Matokeo ya leo yameshuhudia Simba SC ikiibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate FC, ushindi ambao umeifanya iendelee kusalia katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi. Hata hivyo, ushindi huo haujatosha kuziba pengo dhidi ya vinara wa ligi, Yanga SC.

Yanga wameendelea kushikilia kilele cha msimamo kwa kuongoza na alama 44 baada ya kucheza mechi 18, wakiacha pengo la alama tano dhidi ya watani zao wa jadi Simba wenye alama 39 baada ya idadi sawa ya mechi. Tofauti hiyo sasa inaiweka Yanga katika nafasi nzuri ya kutetea ubingwa kwa msimu wa tano mfululizo kama watafanya vizuri katika mechi 12 zilizobaki.

Katika nafasi ya tatu, Azam FC wanaendelea kujikita wakiwa na alama 34 baada ya mechi 18, huku JKT Tanzania wakishika nafasi ya nne kwa alama 29, pia baada ya kucheza mechi 18.

Kwa mtazamo wa ushindani wa ubingwa, unaweza kusema safari ya Yanga kuelekea kutwaa ubingwa wa tano mfululizo iko mikononi mwao.

Katika mechi 12 zilizobaki, Wananchi watahitaji kushinda angalau mechi 10 ili kujihakikishia ubingwa huo, huku wakilazimika kuepuka kupoteza mechi muhimu dhidi ya wapinzani wao wakuu Simba na Azam FC.

Kadri ligi inavyoelekea ukingoni, presha inaendelea kuongezeka, na kila pointi itakuwa na uzito mkubwa katika kuamua nani ataibuka bingwa wa msimu huu wa 2025/2026.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.