Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba SC, Ahmed Ali, amethibitisha kuwa uongozi wa klabu umefikia uamuzi wa kumrudisha mshambuliaji huyo kwenye programu ya vijana baada ya kusimamishwa kutokana na tuhuma za utovu wa nidhamu.
Kwa mujibu wa klabu, Sowah alisimamishwa akiwa kambini mwezi Machi wakati timu ilipokuwa Dodoma ikijiandaa na mchezo wa ligi dhidi ya Dodoma Jiji FC, baada ya malalamiko kutoka kwenye benchi la ufundi kuhusu mienendo yake isiyoridhisha.
“Jonathan Sowah tulimsimamisha kutoka kambi yetu mwezi wa tatu tulipokuwa Dodoma kucheza mechi ya ligi dhidi ya Dodoma Jiji,” alisema Ahmed Ali.
“Alikuwa akituhumiwa kwa makosa kadhaa ya utovu wa nidhamu ambayo yalitokana na malalamiko kutoka benchi la ufundi. Baadaye alirejeshwa Dar es Salaam kusubiri taratibu za klabu zikamilike.”
Ahmed alieleza kuwa baada ya shauri hilo kupelekwa katika Kamati ya Nidhamu ya klabu, mchezaji huyo alipatikana na hatia na kupewa adhabu mbili kuu.
“Adhabu ya kwanza ni faini, na ya pili ni kuamrishwa kufanya mazoezi na timu ya vijana kama sehemu ya malezi na marekebisho ya tabia,” alifafanua.
Kwa sasa, Sowah atakuwa akifanya mazoezi na kikosi cha U20 cha Simba kama sehemu ya uangalizi maalum, huku akitarajiwa kurejea katika timu ya wakubwa endapo ataonyesha mabadiliko chanya ya kitabia na nidhamu.
“Akionyesha mabadiliko mazuri ataunganishwa tena na timu ya wakubwa kuendelea na majukumu yake,” aliongeza Ahmed Ali.
Wakati klabu ikitangaza hatua hiyo ya kinidhamu, taarifa za ndani zinaeleza kuwa Sowah naye amewasilisha barua kwa uongozi akiomba kusitishwa kwa mkataba wake kwa makubaliano ya pande mbili.
Mchezaji huyo amepinga tuhuma zote za utovu wa nidhamu dhidi yake akisisitiza kuwa hakuwa na makosa.



