Mechi ya kiporo ya mzunguko wa 17 wa NBC Premier League inatarajiwa kuchezwa kesho Jumatano, Aprili 15 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Stadium, ambapo Fountain Gate FC watawakaribisha Simba SC katika mchezo unaotarajiwa kuwa na presha kubwa kwa pande zote mbili.
Mchezo huo utaanza saa 10:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki, ukiwa ni miongoni mwa michezo muhimu inayoendelea kuchagiza mbio za ubingwa na pia vita ya kubaki kwenye ligi.
Kwa mujibu wa hali ya msimamo wa ligi kufikia Aprili 14, Simba SC wanashika nafasi ya pili wakiwa na alama 36, huku wakisalia nyuma ya vinara Young Africans SC walio na alama 44. Ushindi katika mchezo huu utawasaidia Wekundu wa Msimbazi kupunguza pengo la pointi na kuendelea kuweka presha katika mbio za ubingwa.
Kwa upande wa Fountain Gate, hali yao si shwari. Timu hiyo inaendelea kupambana kujinusuru na hatari ya kushuka daraja, ikishika nafasi ya 17 baada ya kukusanya alama 16. Hivyo kila mchezo uliosalia unakuwa wa maisha na kifo kwao. Ushindi au hata sare katika mchezo huu unaweza kuwa msaada mkubwa katika kampeni yao ya kubaki ligi kuu.
Simba SC wanaingia uwanjani wakiwa na lengo moja kuu, kupata pointi tatu muhimu zitakazowasaidia kuendelea kusalia katika mbio za ubingwa, huku wakitegemea ubora wa kikosi chao na uzoefu katika mechi kubwa.
Kwa upande mwingine, Fountain Gate ambayo hivi ilitangaza kumuajiri kocha Fredy Felix Minziro, wanatarajiwa kucheza kwa tahadhari kubwa, wakilenga kuzuia mashambulizi ya Simba na kutafuta nafasi za kushtukiza.
Mchezo huu unatarajiwa kuwa na ushindani mkali, ukiwa na uzito mkubwa zaidi kwa Simba katika harakati zao za ubingwa, huku Fountain Gate wakipigania maisha yao ya ligi kuu.



