Basi la timu lavamiwa na majambazi Ghana, mchezaji auawa

Joel JJ By Joel JJ β€’ 13th April 2026


Basi la timu lavamiwa na majambazi Ghana, mchezaji auawa

Tasnia ya soka nchini Ghana imekumbwa na msiba mzito kufuatia kifo cha mchezaji chipukizi Dominic Frimpong, aliyefariki dunia baada ya kushambuliwa kwa risasi katika tukio la ujambazi lililolenga basi la timu yake.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari vya kimataifa, tukio hilo lilitokea Jumapili, Aprili 12, 2026, wakati timu ya Berekum Chelsea ikirejea kutoka mchezo wa Ligi Kuu Ghana dhidi ya Samartex.

Inaelezwa kuwa watu wenye silaha walivamia basi hilo njiani na kuanza kufyatua risasi, hali iliyosababisha taharuki kubwa miongoni mwa wachezaji na viongozi wa timu hiyo. Katika tukio hilo, Frimpong alipigwa risasi kichwani na baadaye alifariki dunia alipokuwa akipatiwa matibabu hospitalini.

Frimpong, aliyekuwa na umri wa miaka 20, alikuwa akiichezea Berekum Chelsea kwa mkopo akitokea Aduana FC. Katika msimu huu, alikuwa amecheza mechi kadhaa na kuonyesha kiwango kizuri kilichomfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wanaochipukia nchini humo.

Shirikisho la Soka Ghana (GFA) limelaani tukio hilo na kutoa salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu, klabu pamoja na wadau wa soka nchini humo.

Tukio hilo pia limeibua hofu kuhusu usalama wa timu za soka wakati wa safari za kwenda na kurejea kwenye mechi za ligi, huku mamlaka zikiahidi kufanya uchunguzi na kuwabaini wahusika wa shambulio hilo.

Kifo cha Frimpong kimeacha pengo kubwa katika soka la Ghana, huku mashabiki na wadau mbalimbali wakiendelea kutoa pole na kutaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya wahusika wa tukio hilo.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.