Simba na Chobwedo kimeeleweka

Joel JJ By Joel JJ • 13th April 2026


Simba na Chobwedo kimeeleweka

Klabu ya Simba SC ya Dar es Salaam inaripotiwa kuwa katika hatua za mwisho kukamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji wa TRA United, Ramadhan Salum Ramadhan maarufu kama “Chobwedo”, kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya uongozi wa klabu hiyo, Simba imefanikiwa kushinda ushindani wa klabu kadhaa zilizokuwa zikimwania mchezaji huyo kutokana na kiwango chake bora alichokionesha msimu huu.

Chobwedo alionesha ubora wake zaidi katika mchezo wa ligi uliopita kati ya TRA United na Simba uliopigwa katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, ambapo timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana. Katika mchezo huo, kiungo huyo wa ushambuliaji alionesha kasi, ubunifu na uwezo wa kuwatatiza mabeki wa Simba, hali iliyoongeza mvuto kwa mabosi wa klabu hiyo.

Taarifa zinaeleza kuwa Simba SC tayari imeandaa mkataba wa miaka miwili kwa mchezaji huyo, ambapo hatua ya awali ni kusaini makubaliano ya awali (pre-contract) kabla ya kukamilisha usajili wake rasmi.

Uongozi wa Simba umeelezwa kubadili mkakati wake wa usajili kwa msimu ujao, ambapo umedhamiria kukamilisha mikataba ya wachezaji mapema kabla ya msimu kumalizika ili kuimarisha maandalizi ya kikosi.

Simba SC pia imekamilisha usajili wa kiungo Kelvin Nashon, ambaye anacheza kwa mkopo katika klabu ya Pamba Jiji akitokea Singida Black Stars, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha eneo la kiungo kuelekea msimu ujao.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.