Kocha Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, amesema atafanya mabadiliko machache ya kiufundi katika kikosi chake kuelekea mchezo wa hatua ya 16 bora ya Kombe la CRDB dhidi ya Dodoma Jiji, unaotarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Barker amesema mabadiliko hayo yanalenga kuongeza ubunifu wa timu katika kutengeneza nafasi za mabao, hasa kutokana na changamoto ya ukame wa mabao iliyojitokeza katika michezo ya hivi karibuni.
Akizungumza kuelekea mchezo huo, Barker alikiri kuwa timu yake imekuwa ikipata nafasi nyingi lakini imekosa umakini wa kuzitumia ipasavyo.
“Mechi ya mwisho tuliyocheza dhidi ya Dodoma Jiji nafikiri tulikuwa na kiwango bora, haikuwa bahati upande wetu hatukuweza kufunga bao lolote,” alisema.
Kocha huyo aliongeza kuwa hali hiyo haijitokezi kwa mara ya kwanza, akibainisha kuwa Simba SC pia haikufanikiwa kufunga katika mechi mbili za Ligi Kuu Tanzania Bara zilizopita.
“Pia tumecheza mechi mbili za ligi kuu pasipo kufunga bao, tunafahamu changamoto inayotukabili na tunafanya kazi kubwa kwenye uwanja wa mazoezi,” alifafanua.
Barker amesema tayari benchi la ufundi linafanyia kazi marekebisho ya kimkakati yatakayosaidia kuongeza ufanisi wa safu ya ushambuliaji na kuimarisha uwezo wa kutengeneza nafasi.
“Tunahitaji kutengeneza nafasi zaidi ili tuweze kufunga magoli, hivyo tutafanya mabadiliko machache ya kimbinu ambayo naamini yatatupa wigo mpana wa kutengeneza nafasi na kufunga mabao,” alisema.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa wa ushindani mkubwa kutokana na umuhimu wake katika hatua ya mtoano, huku kila timu ikiwania nafasi ya kutinga robo fainali ya michuano hiyo



