Simba yatajwa kumuwania kipa wa timu ya Taifa, Nigeria

Joel JJ By Joel JJ β€’ 10th April 2026


Simba yatajwa kumuwania kipa wa timu ya Taifa, Nigeria

Klabu ya Simba SC imeibuka tena ikihusishwa na harakati za kumwania kipa namba moja wa timu ya taifa ya Nigeria Stanley Nwabali, kuelekea msimu wa 2026/2027.

Nwabali anatajwa kuwa ni chaguo la Kocha Mkuu wa Simba Steve Barker ambaye alipendekeza usajili wake ambapo baada ya mchakato wa kumsajili kukwama, ndio Wekundu hao wa Msimbazi wakamsajili Djibrilla Kassali.

Nwabali ni miongoni mwa makipa wanaofanya vyema barani Afrika, akiwa amejijengea jina kupitia kiwango chake cha juu katika mechi za kimataifa na ligi ya Afrika Kusini. Kipa huyo mwenye umri wa miaka 29 alizaliwa Juni 10, 1996 jijini Lagos, Nigeria, na anatajwa kuwa na sifa zote za kipa wa kisasa.

Akiwa na urefu wa takribani mita 1.96, Nwabali anatajwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuokoa mipira ya hatari (shot-stopping), utulivu chini ya presha pamoja na umahiri katika mikwaju ya penalti, sifa zilizomfanya awe chaguo la kwanza katika kikosi cha Nigeria.

Umaarufu wake ulipaa zaidi katika mashindano ya AFCON 2023, ambapo alicheza nafasi muhimu katika mafanikio ya timu yake kufika hatua za juu za mashindano hayo, akionyesha ubora mkubwa hasa katika mechi zenye ushindani mkubwa.

Kabla ya kuanza kuvuma kimataifa, Nwabali aliwahi kucheza katika vilabu mbalimbali vya nyumbani Nigeria kabla ya kujiunga na Chippa United mwaka 2022. Akiwa hapo, alionyesha kiwango kizuri kilichomuwezesha kuvutia macho ya vilabu vingine barani Afrika.

Kwa sasa Nwabali yupo bila timu tangu Februari 2026 baada ya kuachana na Chippa United, hali inayomfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wanaoweza kupatikana kirahisi sokoni, ingawa gharama zake binafsi zinaweza kuwa changamoto.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, kipa huyo anahitaji mshahara wa dola 15,000 kwa mwezi ili kujiunga na Simba, ikiwa ni zaidi ya fedha alizokuwa akilipwa wakati anaitumikia Chippa United.

Hata hivyo, uzoefu wake wa mechi 34 za kimataifa akiwa na Nigeria, pamoja na wastani mzuri wa kuruhusu mabao chini ya moja kwa kila mchezo, vinamfanya kuwa chaguo linaloweza kuongeza utulivu eneo la lango la Simba hasa katika mashindano ya kimataifa.

Kassali alisaini mkataba wa miezi sita na uwezekano wa kuongezewa mkataba ni mdogo hasa ikizingatiwa pia Mouss Camara nae yuko nje akijiimarisha, anaweza kurejeshwa kama mpango wa kumpata Nwabali utakwama kwa mara nyingine.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.