Jarida la France Football limetangaza rasmi mfumo mpya wa tathmini kwa tuzo ya Ballon d’Or ya mwaka 2026, likibainisha vigezo vinne vikuu vitakavyotumika kuwachuja wachezaji bora duniani.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wagombea wote watapimwa kwa kuzingatia mambo yafuatayo:
Kwanza ni mafanikio ya pamoja na mataji, ambapo ubingwa katika ngazi ya klabu na timu ya taifa utaendelea kuwa msingi mkuu wa ushindani wa tuzo hiyo.
Pili ni kiwango binafsi cha mchezaji, ubora wake uwanjani, uwezo wa kubadilisha matokeo ya mechi na mchango wake wa moja kwa moja katika mafanikio ya timu msimu mzima.
Tatu ni nidhamu na uungwana, ambapo tabia njema ndani na nje ya uwanja itakuwa sehemu muhimu ya tathmini ya mchezaji.
Nne ni uwezo wa kung’ara katika mechi kubwa, hasa fainali na hatua za mtoano, ambapo wachezaji hupimwa zaidi kwa namna wanavyobeba timu katika nyakati za presha kubwa.
Aidha, katika toleo la mwaka 2026, msisitizo mkubwa umewekwa kwa mashindano makubwa zaidi duniani, ukiwemo UEFA Champions League na FIFA World Cup.
Imeelezwa wazi kuwa ni wachezaji watakaoonyesha kiwango cha kipekee katika mashindano hayo mawili pekee watakaokuwa na nafasi halisi ya kutwaa tuzo hiyo kubwa zaidi binafsi katika soka.



