Ligi Kuu ya NBC inaendelea leo raundi ya 18 ambapo mechi mbili zinatarajiwa kupigwa mkoani Singida na Mwanza.
Singida BS inayopitia misukosuko baada ya mfululizo wa matokeo mabaya, itakuwa nyumbani uwanja wa Airtel kuikaribisha KMC ambayo pia inachungulia shimo la kuteremka daraja.
Juzi Singid BS ilitangaza kulifuta benchi la ufundi pamoja kuwakata wachezaji wote mishahara kwa asilimia 40 kufuatia mfululizo wa matokeo yasiyoridhisha.
Timu zote zinakutana zikiwa zimetoka kutimua makocha hali inayofanya mchezo huo kuwa muhimu kwa kila ili kupunguza presha inazozikabili timu hizo.
Mtanange kati ya Singida BS dhidi ya KMC unatarajiwa kupigwa saa 8 mchana na kufuatiwa na mchezo kati ya Pamba Jiji dhidi ya Yanga.
Hii ni mechi nyingine inayotarajiwa kuwa na upinzani mkali hasa kutokana na rekodi zinazokutana.
Pamba Jiji hawajapoteza mchezo uwanja wa nyumbani, leo watakuwa na kazi ngumu ya kuwazuia Wananchi kuondoka na alama tatu.
Yanga wakiwa vinara wa ligi, wanazihitaji alama zote tatu ili kuendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi ambao mpaka sasa wanaongoza kwa tofauti ya alama 6.
Yanga ilitua Mwanza juzi ambapo jana vijana wa kocha Pedro Goncalves wakafanya maandalizi yao ya mwisho katika uwanja wa CCM Kirumba.




