Simba kujipanga upya baada ya sare dhidi ya Azam Fc

Joel JJ By Joel JJ β€’ 6th April 2026


Simba kujipanga upya baada ya sare dhidi ya Azam Fc

Klabu ya Simba SC inapanga mikakati mipya ya kuboresha matokeo yake baada ya sare waliyopata dhidi ya Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex jana.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ali, alisema wazi kuwa matokeo hayo hayakuwa malengo ya timu, lakini wamelazimika kuyakubali huku wakielekeza nguvu kwenye mechi zijazo.

Ahmed alieleza kuwa mchezo ulikuwa na ushindani mkubwa na ubora wa hali ya juu kutoka pande zote mbili, lakini akasisitiza kuwa Simba ilikuwa na nafasi kubwa zaidi ya kuibuka na ushindi kama wangezitumia vizuri nafasi walizotengeneza.

Katika tathmini yake, Ahmed pia aligusia baadhi ya matukio ya uwanjani ambayo aliamini yangetafsiriwa tofauti kwa kuzingatia sheria za mchezo, jambo ambalo lingeweza kubadili mwelekeo wa matokeo.

Hata hivyo, alikiri kuwa kwa ujumla matokeo hayo yanaweza kuchukuliwa kama ya haki kwa pande zote mbili, licha ya maumivu kwa upande wa Simba ambao waliamini walistahili ushindi.

Ahmed amebainisha kuwa wanakwenda kurekebisha makosa yaliyojitokeza ili kuimarisha kikosi chao kuelekea hatua zinazofuata za ligi. Ahmed alisisitiza kuwa bado kuna nafasi kubwa ya kufanya vizuri kutokana na idadi ya mechi zilizosalia.

Mchezo unaofuata kwa Simba ni dhidi ya TRA United ukitarajiwa kupigwa April 09 katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha.

Simba inakabiliwa na mfululizo wa mechi baada ya kukamilisha mchezo huo wa kiporo uliopaswa kupigwa March 14 lakini ukaahirishwa baada ya mvua kubwa kujaza maji uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

April 12 Simba watacheza dhidi ya Dodoma Jiji mchezo wa hatua ya 16 bora kombe la CRDB kabla ya kuhitimisha mechi mbili za ligi dhidi ya Fountain Gate (April 15) na Namungo Fc (April 18) na kisha kuelekea Zanzibar kushiriki kombe la Muungano.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.