Dodoma Jiji yajipanga kuikabili Simba kombe la CRDB

Joel JJ By Joel JJ • 6th April 2026


Dodoma Jiji yajipanga kuikabili Simba kombe la CRDB

Wakati presha ikizidi kupanda kuelekea mchezo wa hatua ya 16 bora ya Kombe la CRDB, kati ya Simba dhidi ya Dodoma Jiji ambao utapigwa Jumapili ya wiki hii, Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji Aman Josiah ameweka wazi dhamira yake ya kuiondosha Simba SC kwenye michuano hiyo.

Baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi Fountain Gate katika mchezo uliopita wa ligi kuu, Josiah amesema kikosi chake kina ari kubwa kuelekea mtanange huo uliopangwa kupigwa uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar es salaam.

Josiah amesema watakuwa na muda wa kuisoma Simba kimbinu na kufanya uchambuzi wa kina ili kuhakikisha wanaweka mikakati yao vyema.

Josiah alibainisha kuwa licha ya Simba kuwa na uzoefu mkubwa na historia nzuri kwenye mashindano hayo, hilo haliwatishi kwani watajipanga vyema.

“Tunaiheshimu Simba, lakini hilo halimaanishi hatuna uwezo wa kushinda. Tunajipanga vizuri na kila mchezaji anatambua majukumu yake uwanjani,” alisema kocha huyo.

Mara ya mwisho Dodoma Jiji ilipokutana na Simba uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma katika mchezo wa ligi kuu, timu hizo zilitoka suluhu ya bila kufungana.

Mchezo wa April 12 ni wa mtoano kwa maana lazima mshindi apatikane ambaye atatinga robo fainali ya kombe la CRDB.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.