Inter Milan imeendeleza ubabe wake katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A) baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 5-2 dhidi ya AS Roma katika mchezo uliochezwa Aprili 5, 2026, kwenye uwanja wa San Siro.
Mchezo huo ulianza kwa kasi kubwa ambapo nahodha Lautaro Martínez aliipatia Inter bao la mapema ndani ya dakika ya kwanza, akionyesha kiwango bora baada ya kurejea kutoka majeruhi. Roma walijipanga upya na kufanikiwa kusawazisha kupitia Gianluca Mancini dakika ya 40.
Hata hivyo, wenyeji walirejesha uongozi kabla ya mapumziko kupitia kiungo Hakan Çalhanolu aliyefunga kwa shuti kali la mbali.
Kipindi cha pili kilishuhudia Inter wakitawala mchezo huo kwa kiwango cha juu zaidi. Martínez aliongeza bao lake la pili dakika ya 52, huku Marcus Thuram akifunga na pia kuchangia pasi za mabao. Nicolò Barella alihitimisha karamu ya mabao kwa kufunga bao la tano.
Roma walipata bao lao la pili kupitia Lorenzo Pellegrini dakika ya 70, lakini halikutosha kuzuia kipigo hicho kizito.
Ushindi huo unaifanya Inter kuendelea kuongoza msimamo wa ligi kwa tofauti ya pointi tisa baada ya kufikisha alama 72, hatua inayowapa matumaini makubwa ya kutwaa ubingwa wa Serie A msimu huu. Kwa upande wa Roma, matokeo hayo yanaongeza presha katika harakati zao za kusaka nafasi ya kushiriki michuano ya UEFA Champions League msimu ujao.



