Klabu ya Tottenham Hotspurs imefanikiwa kumshawishi kocha Muitaliano, Roberto De Zerbi, amekubali kujiunga na timu hiyo kwa mkataba wa muda mrefu wa miaka mitano.
De Zerbi ambaye kwa sasa hana timu tangu alipoondoka Marseille mapema mwaka huu, anachukua mikoba ya kuinoa Spurs, klabu inayopitia kipindi kigumu kwenye Ligi Kuu England.
Hatua ya Spurs kumuajiri kocha huyo imekuja kufuatia kuondoka kwa aliyekuwa kocha wa muda Igor Tudor, aliyeachana na klabu hiyo kwa makubaliano ya pande zote baada ya kuhudumu kwa kipindi kifupi.
De Zerbi ameripotiwa kukubali dili hilo na anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka mitano utakaodumu hadi mwaka 2031.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 46 anatambulika kwa mtindo wake wa soka la kushambulia na kumiliki mpira, aliouonyesha alipokuwa akiinoa Brighton, ambapo aliisaidia timu hiyo kufuzu michuano ya Ulaya kwa mara ya kwanza katika historia yao.
Kwa upande wa Spurs, kipaumbele kikubwa kwa sasa ni kuhakikisha wanabaki ndani ya Ligi Kuu, huku ujio wa De Zerbi ukionekana kama suluhisho la haraka na la muda mrefu kwa changamoto zinazowakabili.
De Zerbi anatarajiwa kuanza kazi mara moja akipewa jukumu la kuinusuru timu hiyo pamoja na kuijenga upya kwa ajili ya ushindani wa misimu ijayo.



