Yanga yatinga fainali Muungano Cup baada ya kuichapa Azam Fc 2-1

Joel JJ By Joel JJ β€’ 25th April 2026


Yanga yatinga fainali Muungano Cup baada ya kuichapa Azam Fc 2-1

Mabingwa watetezi Yanga SC wamefanikiwa kutinga hatua ya fainali ya Kombe la Muungano baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Azam FC katika mchezo wa nusu fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar.

Yanga walionyesha kasi na ubora mkubwa tangu mwanzo wa mchezo, wakitawala sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza na kufanikiwa kupata mabao mawili muhimu yaliyowapa nafasi ya kuongoza mapema.

Bao la kwanza la Yanga lilifungwa na Prince Dube, ambaye alimalizia kwa ustadi pasi safi kutoka kwa Allan Okello. Baada ya bao hilo, Yanga waliendelea kushambulia na kuongeza bao la pili kupitia Maxi Nzengeli, akitumia vyema pasi ya Dube.

Azam FC walionekana kupoteza mwelekeo katika kipindi cha kwanza, huku Yanga wakikosa kutumia nafasi zaidi walizozitengeneza ambazo zingeweza kuongeza idadi ya mabao.

Kipindi cha pili kilikuwa tofauti kidogo, ambapo Azam FC walirudi uwanjani wakiwa imara zaidi na kuanza kushambulia kwa tahadhari kubwa. Yanga kwa upande wao walilazimika kucheza kwa nidhamu zaidi wakilinda uongozi wao wa mabao mawili.

Juhudi za Azam FC zilizaa matunda kupitia Feisal Salum, ambaye alifunga bao la kufutia machozi na kurejesha matumaini kwa timu yake, ingawa halikutosha kubadili matokeo ya mwisho.

Matokeo hayo yameiwezesha Yanga SC kusonga mbele hadi fainali ya Kombe la Muungano, ambapo sasa watasubiri mshindi kati ya Simba SC na Mlandege FC katika nusu fainali nyingine itakayopigwa kesho Jumapili.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.