Klabu ya Yanga imewataka mashabiki wake kujitokeza kwa wingi katika uwanja wa KMC Complex kesho Jumamosi, Aprili 11, kuipa sapoti timu hiyo itakapovaana na TMA Stars katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la CRDB.
Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, alisema klabu hiyo inalenga kushinda mchezo huo ili kutinga hatua ya robo fainali na kuendeleza rekodi yao ya kutopoteza mechi katika mashindano hayo kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo.
“Tuna miaka mitano sasa hatujapoteza mchezo kwenye Kombe la Shirikisho la CRDB. Ninaamini rekodi hii inakwenda kutuongezea nguvu ya kupambana katika mchezo dhidi ya TMA Stars,” alisema Kamwe.
Kamwe aliongeza kuwa mchezo huo utapigwa saa 12:30 jioni katika uwanja wa KMC Complex na akawataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu yao katika hatua hiyo muhimu ya mashindano.
“Muda wa mechi ni saa 12:30 jioni na itapigwa pale KMC Complex. Kwa mwanachama na shabiki wa Yanga huna sababu ya kukosa uwanjani kesho kwani mchezo ni wa hatua muhimu ya 16 bora,” alisema.
Akiendelea kuhamasisha, Kamwe alisisitiza umuhimu wa mashabiki kuwa sehemu ya timu, akisema mchezo huo unahitaji hamasa kubwa kutokana na ushindani wake.
“Njoo wewe, rafiki yako na familia yako mje mpate burudani. Hii si mechi ya kawaida kwa sababu ni hatua ya 16 bora. Tumeona Kombe la CRDB limetoa matokeo yasiyotarajiwa kwenye baadhi ya mechi,” alisema.
Yanga inaingia kwenye mchezo huo ikilenga kusonga mbele na kuendeleza rekodi yao nzuri katika mashindano ya CRDB Federation Cup, huku wakitarajia changamoto kutoka kwa TMA Stars ambao nao wanaisaka rekodi ya kutinga robo fainali kwa mara ya kwanza.



