Yanga yaifumua Mbeya City 6-0

Joel JJ By Joel JJ β€’ 16th April 2026


Yanga yaifumua Mbeya City 6-0

Klabu ya Young Africans SC imeendeleza ubabe wake katika Ligi Kuu ya NBC baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 6-0 dhidi ya Mbeya City FC katika mchezo uliochezwa Uwanja wa KMC Complex.

Katika mchezo huo, Yanga walionyesha kiwango cha juu tangu mwanzo hadi mwisho, wakimaliza kazi mapema kwa kufunga mabao matano ndani ya kipindi cha kwanza.

Mshambuliaji Prince Dube alirejea kikosini na kufunga mabao mawili, akifungua pazia la mabao na kufunga bao la sita, ikiwa ni kurejea kwa mafanikio baada ya kukosa baadhi ya michezo kutokana na majeraha.

Mabao mengine yalifungwa na Pacome Zouzoua aliyefunga mawili, huku Maxi Nzengeli na Mohamed Hussein wakiongeza bao moja kila mmoja.

Safu ya ulinzi ya Yanga iliyoongozwa na nahodha Bakari Mwamnyeto ilikuwa imara muda wote wa mchezo, ikiizuia Mbeya City kupata nafasi za hatari, huku kipa Hussein Masalanga akifanya kazi yake bila presha kubwa.

Kwa ushindi huo, Yanga wamefikisha alama 47 kileleni mwa msimamo wa ligi na kuongeza pengo la pointi nane dhidi ya wapinzani wao wa karibu.

Katika mchezo mwingine uliochezwa mapema, Mashujaa FC walilazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Singida Black Stars, katika pambano lililoshuhudiwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Nchemba.

Matokeo hayo yanaendelea kuifanya Yanga kujikita kileleni huku ushindani wa ligi ukiendelea kupamba moto kadri msimu unavyoelekea ukingoni.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.