Yanga yaanza mikakati ya kusukwa upya

Joel JJ By Joel JJ β€’ 4th June 2026


Yanga yaanza mikakati ya kusukwa upya

Wakati mashabiki wa Yanga SC wakiendelea kusubiri hitimisho la msimu huu, uongozi wa klabu hiyo tayari umeanza maandalizi ya awali ya kusuka upya kikosi kitakachoshiriki msimu ujao wa mashindano ya ndani na kimataifa.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa mabingwa hao wa Tanzania Bara wameanza michakato ya awali ya usajili, wakilenga kufanya maboresho makubwa zaidi ili kuhakikisha kila nafasi muhimu inapata mchezaji mwenye ubora unaotakiwa.

Baada ya kutofanya vyema katika dirisha kubwa la usajili lililopita, safari hii Yanga imepanga kuingia sokoni kwa umakini mkubwa zaidi, ikiwa na mpango wa kuhakikisha kila usajili unakuwa na tija kwa kikosi cha benchi la ufundi.

Chanzo kutoka ndani ya uongozi kimeeleza kuwa klabu hiyo inatarajia kufanya mabadiliko makubwa katika idara ya wachezaji wa kigeni, ambapo nyota wasiopungua saba wanatajwa kuwa kwenye mipango ya kutua Jangwani mara dirisha la usajili litakapofunguliwa rasmi.

Iwapo mpango huo utatekelezwa kama ulivyopangwa, itamaanisha kuwa kati ya wachezaji 12 wa kigeni waliopo kwa sasa, ni watano pekee watakaosalia ndani ya kikosi cha msimu ujao, huku wengine wakitarajiwa kuachana na klabu hiyo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kumaliza mikataba au kutokuwa kwenye mipango ya benchi la ufundi.

Kwa sasa, Yanga tayari imeanza mchakato wa kusafisha kikosi chake kwa kuachana na baadhi ya wachezaji waliokuwa wametolewa kwa mkopo katika klabu mbalimbali. Taarifa zinaeleza kuwa kiungo Mohamed Doumbia, Celestin Ecua, Jonathan Ikangalombo pamoja na Moussa Balla Conte hawatakuwa sehemu ya mipango ya Yanga msimu ujao, baada ya uongozi kuamua kutoendelea nao.

Mbali na wachezaji hao waliokuwa kwa mkopo, benchi la ufundi pia linatarajiwa kufanya tathmini ya mwisho kwa baadhi ya nyota waliopo kikosini kwa sasa. Wale ambao hawataingia kwenye mipango ya msimu ujao wataachwa ili kupisha usajili mpya.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.