Klabu ya FC Barcelona imethibitisha kuwa nyota wake kijana, Lamine Yamal (18), atakosa mechi zote zilizosalia za msimu huu baada ya kupata jeraha la misuli ya mguu wa kushoto.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya klabu hiyo, vipimo vya kitabibu vilivyofanyika baada ya mchezo wa La Liga dhidi ya Celta Vigo vilibaini kuwa Yamal amepata jeraha katika misuli ya biceps femoris, sehemu ya nyuma ya paja la mguu wa kushoto.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mchezaji huyo atalazimika kupumzika kikamilifu ili kupona, hatua inayomaanisha hatoshiriki tena katika mechi yoyote ya msimu huu wa 2025/2026.
Kutokuwepo kwa Yamal ni pigo kwa FC Barcelona katika kipindi muhimu cha mwisho wa msimu, ambapo klabu hiyo inakaribia kutwaa ubingwa wa La Liga ikihitaji kushinda michezo angalau michezo mitatu kati ya sita iliyosalia.
Yamal amekuwa miongoni mwa wachezaji muhimu wa kikosi hicho msimu huu, akichangia mabao na pasi za mwisho katika mechi kadhaa muhimu, huku akionekana kuwa moja ya vipaji vikubwa vinavyoibukia Ulaya.
Licha ya majeraha hayo, taarifa zinaeleza kuwa matarajio ya klabu na timu ya taifa ni kuona Yamal akirejea akiwa fiti kabisa kwa ajili ya majukumu ya kimataifa na timu ya taifa ya Hispania.
Mchezaji huyo anatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Spain kitakachoshiriki katika maandalizi na hatimaye fainali za FIFA World Cup 2026 zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico.



