Klabu ya Wolverhampton Wanderers (Wolves) imethibitishwa rasmi kushuka daraja kutoka Premier League baada ya matokeo ya michezo ya Aprili 20, 2026 kuondoa kabisa matumaini yao ya kubaki ligi kuu.
Hatua hiyo imekuja kufuatia sare ya bila kufungana kati ya West Ham United na Crystal Palace, matokeo yaliyofanya tofauti ya pointi kati ya Wolves na nafasi salama kuwa kubwa zaidi ya idadi ya michezo iliyosalia.
Wolves walikuwa mkiani mwa msimamo wa ligi wakiwa na pointi 17 baada ya kucheza michezo 33, wakibakiwa na mechi tano pekee ambazo hata kama wangeshinda zote, wasingeweza kufikia alama za timu zilizo juu yao.
Msimu wa 2025/26 umekuwa mgumu kwa Wolves, ambao walishindwa kushinda katika michezo yao ya mwanzo kwa muda mrefu na kushindwa kujinasua kutoka eneo la kushuka daraja katika kipindi chote cha msimu. Matokeo duni, pamoja na ukosefu wa uthabiti kikosini, vimetajwa kuwa sababu kuu ya anguko hilo.
Kushuka huku kunahitimisha safari ya Wolves ya takriban miaka minane katika Ligi Kuu tangu walipopanda daraja mwaka 2018, ambapo waliwahi kung’ara kwa kumaliza katika nafasi za juu za msimamo na kushiriki mashindano ya Ulaya.



