Hatua muhimu imeanza kuchukuliwa katika kuimarisha miundombinu ya michezo nchini Tanzania baada ya kuanza rasmi kwa ukarabati mkubwa wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, ukiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea michuano mikubwa ya Mataifa ya Afrika, AFCON 2027.
Maboresho hayo yanahusisha eneo la kuchezea (pitch), ambapo kazi ya kubadilisha na kuboresha nyasi inalenga kufikia viwango vya kimataifa vinavyotakiwa na mashirikisho ya soka duniani. Kwa mujibu wa ratiba ya ukarabati, shughuli hizi zinatarajiwa kuchukua takribani miezi sita kukamilika.
Kutokana na mchakato huo, uwanja huo hautatumika kwa shughuli zozote za michezo katika kipindi chote cha ukarabati ili kuruhusu nyasi mpya kustawi na kuimarika ipasavyo.












