Rais wa Marekani, Donald Trump, ameibua mjadala mpya kuhusu bei za tiketi za michuano ya Kombe la Dunia 2026, akizielezea kuwa ni kubwa kupita kiasi na zisizowiana na uwezo wa mashabiki wa kawaida.
Akizungumza katika mahojiano na vyombo vya habari, Trump amesema haelewi sababu ya tiketi hizo kuuzwa kwa bei za juu kiasi hicho, akisisitiza kuwa hata yeye binafsi asingekuwa tayari kulipa gharama hizo ili kushuhudia mechi.
“Singeweza kulipa hizo bei, kusema kweli,” alinukuliwa Trump akisema, kauli iliyozua mjadala mpana kuhusu uhalisia wa gharama za mashindano hayo.
Kombe la Dunia 2026 litakalofanyika kwa pamoja nchini Marekani, Canada na Mexico, limekuwa likikabiliwa na malalamiko kutoka kwa mashabiki na wadau wa soka kuhusu mfumo wa bei unaotumika, unaojulikana kama dynamic pricing, ambapo tiketi hupanda bei kulingana na mahitaji.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, baadhi ya tiketi za mechi za awali zimeuzwa kwa zaidi ya dola 1,000, huku mechi kubwa zikienda hadi maelfu ya dola, hali inayoibua hofu kuwa mashabiki wa kawaida wanaweza kushindwa kumudu kuhudhuria.
Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limeendelea kutetea mfumo huo, likisema bei zinaendana na thamani ya tukio na mahitaji makubwa ya kimataifa ya mashindano hayo, ambayo yanatarajiwa kuvunja rekodi ya mahudhurio.
Wakati mjadala huo ukiendelea, wadau mbalimbali wa soka wameitaka FIFA kufanya tathmini ya bei hizo ili kuhakikisha mashabiki wengi zaidi wanapata nafasi ya kushuhudia moja ya michuano mikubwa zaidi duniani.
Kombe la Dunia 2026 linatarajiwa kuanza Juni 2026, likiwa na mvuto mkubwa kimataifa lakini pia likigubikwa na mjadala mkali kuhusu gharama za tiketi.



