Klabu ya Real Madrid imewachukulia hatua kali viungo Aurélien Tchouaméni na Federico “Fede” Valverde kwa kuwatoza faini ya Euro 500,000 kila mmoja, sawa na zaidi ya Sh1.5 bilioni za Tanzania, kufuatia tukio la kinidhamu lililotokea ndani ya klabu hiyo.
Hatua hiyo imekuja baada ya wawili hao kuingia kwenye mzozo mkubwa uliotajwa kuzua taharuki ndani ya kikosi cha Real Madrid wakati wa mazoezi katika kituo cha Valdebebas, jijini Madrid.
Kwa mujibu wa taarifa, ugomvi huo ulianzia mazoezini baada ya kuchezeana faulo kali kabla ya kuendelea hadi kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
Ripoti hizo zinaeleza kuwa hali ilihitaji viongozi wa benchi la ufundi pamoja na baadhi ya wachezaji kuingilia kati ili kutuliza vurugu hizo.
Licha ya uzito wa tukio hilo, Real Madrid imeamua kutowasimamisha nyota hao kucheza mechi zijazo baada ya wote wawili kuwasilisha maombi rasmi ya radhi kwa viongozi wa klabu, benchi la ufundi pamoja na wachezaji wenzao.
Chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo kimeeleza kuwa uongozi wa Madrid umechukua hatua hiyo kama sehemu ya kulinda nidhamu na heshima ya klabu.
“Hakuna mchezaji aliye juu ya sheria ndani ya Real Madrid. Nidhamu ni msingi wa mafanikio ya klabu hii,” kilieleza chanzo hicho.
Faini hiyo inatajwa kuwa miongoni mwa adhabu kubwa zaidi za kifedha kuwahi kutolewa ndani ya klabu hiyo kwa kosa la kinidhamu.
Tukio hilo limezua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki wa soka duniani, huku baadhi wakisifu uamuzi wa klabu kuchukua hatua kali, wakati wengine wakishangazwa na uamuzi wa kutowasimamisha kucheza.
Hata hivyo, viongozi wa Real Madrid wanaamini suala hilo limefungwa rasmi baada ya wachezaji hao kuonyesha majuto na kuahidi kutorudia kosa hilo.



