Klabu ya Simba SC imeonyesha ubora mkubwa na kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la CRDB baada ya kuichapa TRA United mabao 4-0 katika mchezo wa robo fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex.
Simba ilianza mchezo huo kwa kasi kubwa huku ikifanikiwa kupata bao la mapema dakika ya tano kupitia kiungo mshambuliaji Clatous Chama ‘Mwamba wa Lusaka’ aliyemalizia kwa ustadi krosi safi kutoka kwa Nickson Kibabage.
Bao hilo limeendelea kuthibitisha kiwango bora cha Chama ambaye sasa amefunga mabao sita katika michezo mitano mfululizo akiwa katika kiwango cha juu cha kuzitikisa nyavu.
Baada ya bao hilo, Simba iliendelea kulitawala dimba kwa kucheza soka la kushambulia huku TRA United wakionekana kushindwa kuhimili presha ya wekundu hao wa Msimbazi.
Alikuwa ni kiungo mshambuliaji Anicet Oura aliiongezea Simba bao la pili kwa shuti kali la mbali lililotokana na pasi ya Alassane Kante, na kufanya Simba kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili kocha wa Simba, Steve Barker, alifanya mabadiliko kadhaa kwa kuwatoa Clatous Chama na Oura huku akiwaingiza Suleiman Mwalimu pamoja na Inno Loemba ili kuongeza nguvu mpya kikosini.
Mabadiliko hayo yalizaa matunda baada ya Suleiman Mwalimu kuandika bao la tatu kwa kuunganisha krosi nzuri ya David Kameta ‘Duchu’ ambaye alikuwa na kiwango bora na kufanikiwa kutoa asisti mbili katika mchezo huo.
Kinda Bashiri Kibaila naye alijitokeza kuhitimisha karamu ya mabao kwa kufunga bao la nne lililoweka muhuri wa ushindi mnono kwa Simba.
Kutokana na ushindi huo, Simba sasa imefuzu hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ambapo itakutana na Coastal Union katika pambano linalotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Ushindi huo pia unaendelea kuonyesha dhamira ya Simba kupigania kutwaa taji la CRDB Cup msimu huu huku safu yao ya ushambuliaji ikiendelea kuwa tishio kwa wapinzani.



