Ligi Kuu ya NBC inaendelea leo ambapo mechi mbili zinapigwa mkoani Arusha na Manyara.
Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha kutakuwa na mchezo wa kukata na shoka wenyeji TRA United wakiikaribisha Simba.
Ni mchezo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka mkoani humo hasa ikizingatiwa mchezo huo awali ulipaswa kupigwa March 14 lakini uliahirishwa baada ya mvua kubwa kunyesha na kupelekea kujaza maji uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Wekundu wa Msimbazi wanazihitaji alama zote tatu ili kupunguza gap dhidi ya watani zao Yanga ambao ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Pamba Jiji jana umewafanya wajiimarishe kileleni kwa tofauti ya alama 9.
TRA United wametamba kuwa hakuna timu itatoka salama uwanja wa Sheikh Amri Abeid baada ya kuifunga Singida BS mabao 2-0 katika mchezo uliopita kwenye uwanja huo.
Ikumbukwe pia hata vinara wa ligi Yanga waliacha alama mbili Arusha baada ya kutoka suluhu ya bila kufungana.
Mchezo mwingine utapigwa kule Manyara kati ya Mbeya City dhidi ya Azam Fc. Huu ni mchezo muhimu kwa kila upande Mbeya City nao wakihitaji alama zote tatu ili kujiweka eneo salama na hatari ya kushuka daraja huku Azam Fc wakitambua kama wanakosa ushindi katika mchezo huo, pengine matumaini ya kuwania ubingwa msimu huu yatazidi kufifia.




