Miaka 10 ya kusubiri imefika tamati, baada ya Mamelodi Sundowns kutwaa taji lao la pili la CAF Champions League kufuatia sare ya mabao 1-1 dhidi ya AS FAR katika mchezo wa marudiano wa fainali uliopigwa Rabat, Morocco. Sundowns walitwaa ubingwa huo kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1 baada ya kushinda mchezo wa kwanza kwa bao 1-0 mjini Pretoria.
Bao la AS FAR lilifungwa kwa mkwaju wa penalti kupitia nahodha Mohamed Hrimat kipindi cha kwanza na kufanya mchezo kuwa mgumu kwa Sundowns. Hata hivyo, kiungo Teboho Mokoena aliibuka shujaa kwa kufunga bao muhimu dakika za mwisho kipindi cha kwanza na kurejesha matumaini ya wababe hao wa Afrika Kusini.
Kipa Ronwen Williams naye alikuwa nguzo muhimu baada ya kuokoa penalti nyingine ya Hrimat mwishoni mwa mchezo na kuhakikisha Sundowns wanabeba taji hilo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2016.
Ubingwa huo umefuta maumivu ya misimu kadhaa ambayo Sundowns walikuwa wakigonga mwamba hatua za mwisho za mashindano hayo. Tangu walipotwaa taji lao la kwanza mwaka 2016 kwa kuifunga Zamalek ya Misri, klabu hiyo imeendelea kuwa miongoni mwa timu bora Afrika lakini ikishindwa kufika kileleni tena kwa karibu muongo mmoja. Mwaka jana walifika fainali lakini wakapoteza dhidi ya Pyramids FC ya Misri kwa jumla ya mabao 3-2.
Safari ya Sundowns kuelekea ubingwa wa mwaka huu ilikuwa ya kuvutia. Waliondoa vigogo mbalimbali akiwemo Esperance de Tunis katika nusu fainali huku AS FAR wakitinga fainali baada ya kuwatoa RS Berkane.
Kocha Miguel Cardoso pia ameandika historia yake binafsi baada ya kushinda taji hilo kwa mara ya kwanza, ikiwa ni baada ya kupoteza fainali mbili za awali katika michuano ya CAF. Ushindi huu pia umeihakikishia Sundowns nafasi ya kushiriki michuano ya Intercontinental Cup pamoja na Kombe la Dunia la Klabu mwaka 2029.
Kwa ushindi huo, Mamelodi Sundowns sasa wanaungana na vilabu vikubwa vya Afrika vilivyowahi kutwaa taji la CAF Champions League zaidi ya mara moja, huku wakirejesha heshima ya soka la Afrika Kusini katika ramani ya bara hilo. Mashabiki wao maarufu kama “Masandawana” sasa wana kila sababu ya kusherehekea baada ya miaka 10 ya subira, maumivu na matumaini yasiyokata tamaa.



