Baada ya msimu mgumu uliowaweka karibu na eneo la kushuka daraja, Tottenham Hotspur wameanza harakati za kurejesha makali yao kwa kuangalia soko la usajili mapema, wakilenga kuimarisha safu ya ushambuliaji kuelekea msimu ujao.
Kwa mujibu wa mwanahabari wa usajili wa soka, Fabrizio Romano, Spurs wamefufua tena nia yao ya kumsajili winga wa Brazil, Savinho, ambaye kwa sasa anaitumikia Manchester City.
Romano ameripoti kuwa Tottenham wanamfuatilia tena Savinho katika dirisha la usajili la kiangazi, baada ya mazungumzo ya awali kuvunjika mwaka 2025. Winga huyo alikuwa karibu kujiunga na Spurs mwaka mmoja uliopita, lakini Manchester City walizuia uhamisho huo.
Hata hivyo, hali ya sasa inaonyesha kuwa uwezekano wa kuondoka kwake Etihad uko wazi zaidi, huku mazungumzo ya awali kati ya pande husika yakianza tena. Inasemekana Savinho mwenyewe yuko tayari kwa changamoto mpya na anavutiwa na mradi wa Tottenham unaoendelea kujengwa upya.
Zaidi ya Spurs, klabu ya Newcastle United pia inaripotiwa kumfuatilia kwa karibu winga huyo wa Brazil, jambo linaloongeza ushindani katika mbio za kumsaini.
Ripoti hizo pia zinaeleza kuwa kocha Roberto De Zerbi anavutiwa sana na Savinho, akimuhitaji katika kikosi chake ambacho msimu ulioisha kimemaliza nafasi ya 17.



