Sowah na Simba mwisho umefika

Joel JJ By Joel JJ β€’ 9th April 2026


Sowah na Simba mwisho umefika

Mshambuliaji wa Simba SC Jonathan Sowah, amewasilisha barua rasmi kwa uongozi wa klabu hiyo akiomba kuvunja mkataba wake, kufuatia mgogoro wa kinidhamu unaomkabili.

Taarifa za ndani zinaeleza kuwa hatua hiyo imekuja baada ya mchezaji huyo kusimamishwa na klabu kutokana na tuhuma za utovu wa nidhamu. Awali, Sowah alipewa nafasi ya kujitetea huku uongozi ukisubiri kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu hatma yake.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Sowah ambaye amefunga mabao matatu msimu huu, anapinga tuhuma zinazomkabili na amependekeza mkataba wake uvunjwe kwa makubaliano ya pande zote mbili.

Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Simba, imethibitisha kuwa tayari mchezaji huyo amechukua hatua rasmi kutaka kuachana na klabu hiyo.

Inaelezwa kuwa hata kabla ya ombi hilo, uongozi wa Simba ulikuwa unaelekea kwenye uamuzi wa kutomrejesha mchezaji huyo kikosini kutokana na mwenendo wake wa kinidhamu.

Sowah alijiunga na Simba akitokea Ghana akiwa na matarajio makubwa kutoka kwa mashabiki, lakini changamoto za nidhamu zimeonekana kuathiri safari yake ndani ya kikosi hicho.

Hadi sasa, uongozi wa Simba haujatoa tamko rasmi kuhusu hatma ya mchezaji huyo, lakini ni wazi Sowah hatarajiwi kuendelea kuwa sehemu ya kikosi cha Simba.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.