Mshambuliaji wa Simba, Jonathan Sowah, ameripotiwa kuwa katika wakati mgumu ndani ya klabu hiyo baada ya mvutano kati yake na uongozi kufuatia masuala ya utovu wa nidhamu.
Sowah alipatikana na hatia ya makosa ya kinidhamu, jambo lililosababisha uongozi wa Simba kumchukulia hatua za kinidhamu kumtaka arejee mazoezini kwa muda akiwa na timu ya vijana kabla ya kurejeshwa kwenye kikosi cha kwanza.
Hata hivyo, mshambuliaji huyo wa Ghana alikaidi maelekezo hayo, hatua ambayo imezidi kuzorotesha uhusiano wake na uongozi wa klabu ya Msimbazi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescentius Magori, alithibitisha kuwepo kwa hatua za kinidhamu dhidi ya mchezaji huyo akieleza kuwa hatma yake itafahamika mwishoni mwa msimu.
“Baada ya kupatikana na hatia kwenye makosa ya utovu wa nidhamu yaliyokuwa yanamkabili, Kamati ikatoa uamuzi wa adhabu kama ilivyoelekezwa mwanzo,” alisema Magori.
Aliongeza: “Sowah alipaswa kwenda kufanya mazoezi na timu ya vijana akagoma. Ukigoma kwenda huko basi tunaangalia kwenye kanuni za nidhamu kuna adhabu gani, basi tunafanya.”
Ni wazi hatma ya Sowah kuendelea kuitumikia Simba ipo mashakani na huenda akachukuliwa hatua kali zaidi na uongozi wa klabu hiyo.
Sowah alijiunga na Simba akitokea Singida Black Stars katika dirisha lililopita, baada ya mazungumzo ya makubaliano kati ya pande husika.
Hata hivyo, safari yake Msimbazi haijaenda kama ilivyotarajiwa, kwani amehusishwa na matukio kadhaa ya utovu wa nidhamu ambayo yamesababisha akose baadhi ya mechi muhimu za kikosi hicho.



