Michezo miwili ya Ligi Kuu ya NBC imepigwa leo Jumanne, Mei 26, kukamilisha mechi za mzunguuko wa 25.
Katika Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, Tanzania Prisons waliibuka na ushindi muhimu wa mabao 3-1 dhidi ya Pamba Jiji FC, matokeo yaliyoongeza matumaini ya timu hiyo kujinasua kwenye hatari ya kushuka daraja.
Ushindi huo umeifanya Prisons kuendelea kupambana kusalia ndani ya NBC Premier League huku wakionyesha ari mpya katika hatua za mwisho za msimu.
Wakati huo huo mkoani Singida, Singida Black Stars waliendelea na kiwango bora baada ya kuichapa Mbeya City FC mabao 4-1 kwenye Uwanja wa Airtel.
Mbeya City ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao kupitia bao la kujifunga dakika ya nne, lakini Singida Black Stars walirejea kwa nguvu na kusawazisha kupitia Ande Cirille dakika ya 16 kabla ya Malanga Horso Mwaku kufunga bao la pili dakika ya 18. Kipindi cha pili, Khalid Aucho aliongeza bao la tatu kwa mkwaju wa penalti dakika ya 84 kabla ya Malanga kufunga tena dakika ya 89 kuhitimisha ushindi wa mabao 4-1.
Matokeo hayo yameifanya Singida Black Stars kujiimarisha katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi, hatua inayoongeza matumaini yao ya kumaliza msimu kwenye nafasi nzuri ya ushindani wa kimataifa.
Kwa upande mwingine, hali imeendelea kuwa mbaya kwa Mbeya City ambao bado wanabaki kwenye eneo la hatari la kucheza play-off ya kushuka daraja. Kipigo hicho kimeongeza presha kwa timu hiyo kuelekea michezo ya mwisho ya msimu huku mashabiki wakianza kuwa na hofu ya hatma yao kwenye ligi kuu.



