Simba yaunguruma Zanzibar, yatwaa ubingwa Muungano Cup baada ya ushindi dhidi ya Yanga

Joel JJ By Joel JJ β€’ 29th April 2026


Simba yaunguruma Zanzibar, yatwaa ubingwa Muungano Cup baada ya ushindi dhidi ya Yanga

Hatimaye mambo yamebadilika! Simba SC wametwaa ubingwa wa Kombe la Muungano baada ya ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya watani wao wa jadi Yanga SC katika fainali kali iliyochezwa kwenye New Amaan Complex.

Mchezo huo ulikuwa na ushindani mkubwa kwa dakika zote 120, huku timu zote zikionesha ari, nidhamu na mbinu za hali ya juu. Dakika 90 za kawaida zilimalizika kwa suluhu ya bila kufungana, na hata katika muda wa nyongeza mambo yaliendelea kuwa magumu huku kila upande ukisaka bao la ushindi.

Dakika za mwisho kabisa ndipo drama ilipojitokeza. Kiungo mshambuliaji Clatous Chama alifanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari na Edmund John, hali iliyomlazimu mwamuzi kuamuru ipigwe penati. Bila presha, Suleiman Mwalimu aliitumia vyema nafasi hiyo na kufunga bao pekee lililoipa Simba ushindi huo muhimu.

Ulikuwa ushindi uliopatikana kwa jasho na kujituma kwa kiwango cha juu kutoka kwa wachezaji wa Simba, ambao walidhibiti mchezo kwa nidhamu na kupambana hadi dakika ya mwisho. Huu pia ni ushindi unaovunja matarajio ya Yanga waliokuwa na mwendelezo mzuri wa matokeo katika mechi za hivi karibuni.

Kocha Steve Barker pamoja na benchi lake la ufundi wanastahili pongezi kwa mbinu zilizowezesha timu yao kufikia mafanikio haya. Ushindi huu unaashiria mwanzo wa enzi mpya kwa Simba, huku mashabiki wakianza kuamini tena katika ubora wa timu yao.

Katika michuano hiyo pia Simba imechukua tuzo za kipa bora Hussein Abel, Hussein Mbegu akibeba tuzo ya mchezaji bora chipukizi, Rushine de Reuck akibabe tuzo ya mchezaji bora wa mashindano huku Seleman Mwalimu akichukua tuzo ya mfungaji bora wakati kocha bora ni Steve Barker

Kwa kutwaa ubingwa huo, Simba pia imeondoka na kitita cha Tsh Milioni 150 huku Yanga iliyomaliza nafasi ya pili ikiondoka na kitita cha Tsh Milioni 100.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.