Simba yatajwa kumuwania winga Azam Fc

Joel JJ By Joel JJ • 22nd May 2026


Simba yatajwa kumuwania winga Azam Fc

Klabu ya Simba SC imeendelea kujipanga kwa ajili ya msimu ujao kwa kufanya usajili wa wachezaji wa ndani, ambapo tayari imekamilisha mpango wa kumsajili beki wa kulia Nathaniel Chilambo kutoka Azam FC.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya klabu, Chilambo ambaye mkataba wake na Azam FC unatarajiwa kumalizika mwezi ujao, tayari amesaini “pre-contract” ya kuitumikia Simba. Inadaiwa kuwa mchezaji huyo amekubali mkataba wa miaka mitatu na Wekundu wa Msimbazi, hatua inayoashiria mwanzo wa maboresho ya kikosi hicho.

Hata hivyo, Simba haijaishia hapo. Klabu hiyo sasa imemuweka kwenye rada winga wa Azam FC, Abdul Suleiman “Sopu”, ambaye naye mkataba wake unakaribia kufikia ukomo mwezi ujao.

Kama ilivyo kwa Chilambo, Sopu pia anaweza kujiunga na Simba bila ada ya uhamisho endapo mazungumzo yatakamilika baada ya mkataba wake na Azam FC kumalizika.

Sopu ni mchezaji aliyekulia kwenye mfumo wa vijana wa Simba B kabla ya kujiunga na Coastal Union, na baadaye kusajiliwa na Azam FC. Uzoefu huo unamfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wanaoeleweka vyema kwenye soka la Tanzania.

Msimu huu, Sopu hakuonekana sana uwanjani kutokana na changamoto za majeraha, lakini kwa sasa ameonekana kurejea fiti na anapambana kurejesha nafasi yake ndani ya kikosi cha Azam FC.

Simba inaonekana kuendelea na mkakati wa kufunga usajili mapema ili kuhakikisha inakuwa tayari kabla ya dirisha la usajili kufunguliwa rasmi, hatua inayolenga kuimarisha kikosi kwa ajili ya msimu ujao.

Wakati huo huo, taarifa zinaeleza kuwa Simba pia imekaribia kukamilisha usajili wa kiungo Kelvin Nashon kutoka Pamba Jiji FC pamoja na winga Ramadhan Chobwedo kutoka TRA United, ikiwa ni sehemu ya kuongeza kina na ushindani ndani ya timu.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.