Simba SC imefanikiwa kurejea katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kuichapa JKT Tanzania bao 1-0 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo ulikuwa mgumu kwa pande zote mbili, ambapo Simba walionekana kutawala mchezo kwa muda mwingi huku JKT Tanzania wakicheza kwa nidhamu ya hali ya juu ya kujilinda na kutegemea mashambulizi ya kushitukiza.
Licha ya kutengeneza nafasi kadhaa muhimu katika kipindi cha kwanza, Simba walishindwa kuzitumia ipasavyo na iliwabidi kusubiri hadi kipindi cha pili kupata bao la ushindi kupitia kwa Clatous Chama, ambaye aliendelea kuonyesha mchango wake muhimu katika kikosi hicho.
Kiungo mshambuliaji Elie Mpanzu aliendeleza makali yake baada kuandikisha asisti nyingine muhimu, akimtengenezea Chama bao hilo ikiwa ni muendelezo wa ushirikiano wao mzuri kama ilivyoshuhudiwa katika mchezo uliopita dhidi ya Yanga.
Kipindi cha pili JKT Tanzania walionekana kuongeza kasi na kujaribu kurejea mchezoni, lakini Simba waliimarisha safu yao ya ulinzi na kudhibiti mashambulizi hayo hadi mwisho wa mchezo.
Kwa ushindi huo, Simba imefikisha alama 46 na kurejea nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, ikiiangusha Azam FC ambayo sasa imeshuka hadi nafasi ya tatu.



