Simba yamtaka beki Azam Fc

Joel JJ By Joel JJ β€’ 1st May 2026


Simba yamtaka beki Azam Fc

Klabu ya Simba SC imeanza rasmi mazungumzo na mlinzi wa kulia wa Azam FC Nathaniel Chilambo, katika harakati za kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu ujao.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani, Simba imeweka mkazo kwenye eneo la ulinzi wa pembeni, hasa upande wa kulia, ambako kwa sasa kuna nahodha Shomari Kapombe pamoja na David Kameta 'Duchu'.

Hata hivyo, Kameta bado hajafanikiwa kumpa ushindani wa moja kwa moja Kapombe, jambo lililoifanya benchi la ufundi kuona kuna haja ya kuimarisha eneo hilo.

Kocha wa Simba, Steve Barker, ameripotiwa kupendekeza maboresho ya eneo hilo, akitaka timu iwe na chaguo zaidi katika nafasi muhimu za ulinzi.

Inaelezwa kuwa mkataba wa Chilambo na Azam FC unafikia tamati mwishoni mwa msimu huu, hali inayomruhusu mchezaji huyo kuingia kwenye mazungumzo na klabu yoyote inayomuhitaji. Hii imeifanya Simba kuchukua hatua za mapema ili kumnasa beki huyo kabla ya dirisha rasmi la usajili kufunguliwa.

Vyanzo vinaeleza kuwa uongozi wa Simba tayari umeandaa ofa ya mkataba wa miaka miwili, ikiwa ni sehemu ya mpango wa muda mrefu wa kuimarisha kikosi. Endapo makubaliano yatakamilika, Chilambo atasaini mkataba wa awali (pre-contract) kabla ya kujiunga rasmi.

Simba SC pia imeonyesha kubadilisha mkakati wake wa usajili, ambapo sasa inahakikisha inakamilisha mazungumzo mapema kabla ya dirisha la uhamisho kufunguliwa, ili kuepuka ushindani mkali wa soko.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.