Simba yaipigia hesabu kali Tanzania Prisons

Joel JJ By Joel JJ • 9th May 2026


Simba yaipigia hesabu kali Tanzania Prisons

Kikosi cha Simba SC kinaendelea na maandalizi makali kuelekea mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Tanzania Prisons utakaopigwa Jumapili, May 10 katika dimba la KMC Complex jijini Dar es Salaam.

Wekundu wa Msimbazi wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na lengo moja tu la kuhakikisha wanapata alama tatu muhimu katika mbio za kuwania ubingwa wa ligi kuu msimu huu.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuelekea mchezo huo, Kocha Msaidizi wa Simba, Suleiman Matola, amesema maandalizi ya timu yanaendelea vizuri huku wachezaji wote wakiwa katika hali nzuri kuelekea pambano hilo.

“Maandalizi ya mchezo yamekamilika kwa kiasi kikubwa, wachezaji wote wako kwenye hali nzuri kuelekea mchezo huu. Tunajua hautakuwa mchezo mwepesi lakini tumejiandaa kupambana ili kupata alama tatu,” alisema Matola.

Matola ameweka wazi kuwa benchi la ufundi linautambua ubora wa Tanzania Prisons, lakini Simba imejipanga kuhakikisha haitoi nafasi ya kupoteza pointi katika kipindi hiki muhimu cha msimu.

Mchezo huo pia utakuwa wa kwanza kwa Simba kucheza katika uwanja wa KMC Complex kama uwanja wao wa nyumbani msimu huu baada ya kuhamia rasmi kutoka uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni.

Uamuzi wa kurejea KMC Complex umetokana na changamoto za hali ya hewa pamoja na matumizi makubwa ya uwanja wa Isamuhyo katika kipindi hiki cha mvua zinazoendelea jijini Dar es Salaam.

Kwa sasa Simba wanaonekana kuingia kwenye hatua muhimu ya mwisho ya msimu huku kila mchezo ukiwa na uzito mkubwa katika mbio za ubingwa. Mashabiki wa klabu hiyo wanatarajia kuona timu yao ikiendeleza kiwango kizuri na kuendelea kuweka presha kwa wapinzani wao kwenye msimamo wa ligi.

Simba pia wanatarajiwa kucheza mechi zao zote zilizosalia msimu huu katika dimba la KMC Complex huku matumaini yakiwa makubwa ya kumaliza msimu kwa nguvu.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.